Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24

Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 4 Biblia Habari Njema (BHN)

Kujaribiwa kwa Yesu

1. Yesu alitoka mtoni Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani.

2. Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa.

3. Ndipo Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”

4. Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’”

5. Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia,

6. “Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza.

7. Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu.”

8. Yesu akamjibu, “Imeandikwa:‘Utamwabudu Bwana Mungu wako,na kumtumikia yeye peke yake.’”

9. Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa hekalu, akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini

10. kwa maana imeandikwa:‘Atawaamuru malaika wake wakulinde,’

11. na tena,‘Watakuchukua mikononi mwao,usije ukajikwaa mguu kwenye jiwe.’”

12. Lakini Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’”

13. Ibilisi alipokwisha mjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.

Yesu anaanza kazi yake Galilaya

14. Hapo Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani.

15. Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.

Yesu anakataliwa huko Nazareti

16. Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti.

17. Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:

18. “Roho wa Bwana yu juu yangu,kwani ameniweka wakfuniwaletee maskini Habari Njema.Amenituma niwatangazie mateka uhuru wao,na vipofu watapata kuona tena;amenituma niwakomboe wanaoonewa,

19. na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.”

20. Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.

21. Naye akaanza kuwaambia, “Andiko hili mlilosikia limetimia leo.”

22. Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”

23. Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: ‘Mganga jiponye mwenyewe,’ na pia mtasema: ‘Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye pia hapa kijijini mwako.’”

24. Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi kijijini mwake.

25. Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Elia. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.

26. Hata hivyo, Elia hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarefathi katika Sidoni.

27. Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani mwenyeji wa Siria.”

28. Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.

29. Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.

30. Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.

Mtu mwenye pepo mchafu

31. Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu wilayani Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.

32. Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.

33. Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:

34. “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!”

35. Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.

36. Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”

37. Habari za Yesu zikaenea mahali pote katika eneo lile.

Yesu anawaponya watu wengi

38. Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.

39. Yesu akaja akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Yule mama akainuka mara, akawatumikia.

40. Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.

41. Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walijua kwamba yeye ndiye Kristo.

Yesu anahubiri huko Yudea

42. Kesho yake asubuhi, Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta. Hao watu walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao.

43. Lakini yeye akawaambia, “Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo.”

44. Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.