Agano la Kale

Agano Jipya

Ufunuo 12:8-18 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Lakini joka hilo na malaika wake walishindwa, na hatimaye hapakuwa tena na nafasi mbinguni kwa ajili yao.

9. Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani ambaye huudanganya ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja naye.

10. Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: “Sasa umefika ukombozi na nguvu na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake! Maana yule aliyewashtaki ndugu zetu mbele ya Mungu ametupwa chini. Naam, ametupwa chini huyo anayewashtaki usiku na mchana.

11. Ndugu zetu wamemshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno waliloshuhudia; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa.

12. Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba muda wake uliobakia ni mfupi.”

13. Joka lilipotambua kwamba limetupwa chini duniani, likaanza kumwinda yule mama aliyekuwa amejifungua mtoto wa kiume.

14. Lakini mama huyo akapewa mabawa mawili ya tai apate kuruka mbali sana na hilo joka, mpaka mahali pake jangwani ambapo angehifadhiwa salama kwa muda wa miaka mitatu na nusu.

15. Basi, joka likatapika maji mengi kama mto, yakamfuata huyo mama nyuma ili yamchukue.

16. Lakini nchi ikamsaidia huyo mama: Ikajifunua kama mdomo na kuyameza maji hayo yaliyotoka kinywani mwa hilo joka.

17. Basi, joka hilo likamkasirikia huyo mama, likajiondokea, likaenda kupigana na wazawa wengine wa huyo mama, yaani wote wanaotii amri za Mungu na kumshuhudia Yesu.

18. Basi, likajisimamia ukingoni mwa bahari.

Kusoma sura kamili Ufunuo 12