Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22

Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 15 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Abiya wa Yuda

1. Abiya alianza kutawala huko Yuda mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yeroboamu, mwanawe Nebati.

2. Alitawala kwa muda wa miaka mitatu akiwa Yerusalemu. Mama yake alikuwa Maaka binti Absalomu.

3. Abiya alitenda dhambi zilezile alizotenda baba yake, wala hakuwa na moyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama alivyokuwa babu yake Daudi.

4. Hata hivyo, kwa ajili ya Daudi, Mwenyezi-Mungu alimpatia Abiya mwana atakayetawala baada yake, kuwa taa ya kuangaza Yerusalemu na kuuweka imara mji wa Yerusalemu.

5. Mwenyezi-Mungu alifanya hivyo kwa kuwa Daudi alitenda mema mbele yake na hakukiuka aliyomwamuru Mwenyezi-Mungu siku zake zote, isipokuwa tu ule mkasa wa Uria, Mhiti.

6. Kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote alipokuwa mtawala.

7. Matendo mengine ya Abiya, na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Abiya na Yeroboamu waliishi katika hali ya vita.

8. Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na mwanawe Asa akatawala mahali pake.

Asa, mfalme wa Yuda

9. Mnamo mwaka wa ishirini wa utawala wa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, Asa alianza kutawala huko Yuda.

10. Alitawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja. Mama yake alikuwa Maaka, binti Absalomu.

11. Mfalme Asa alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya Daudi babu yake.

12. Aliwafukuza nchini wale wafiraji wa kidini, akaziondoa sanamu zote ambazo babu zake walikuwa wamezitengeneza.

13. Alimvua Maaka, mama yake, cheo chake cha mama malkia, kwa sababu alitengeneza sanamu ya Ashera, mungu wa kike, na hiyo sanamu akaivunjavunja na kuiteketeza kwenye bonde la Kidroni.

14. Lakini mahali pa juu pa kutambikia miungu hapakuharibiwa; hata hivyo, yeye alikuwa na moyo mwaminifu kwa Mwenyezi-Mungu maisha yake yote.

15. Alirudisha nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu vyombo vyote vilivyokuwa vimewekwa wakfu na baba yake, pamoja na vile vyake yeye mwenyewe: Vyombo vya fedha, dhahabu na vyombo vinginevyo.

16. Mfalme Asa wa Yuda, na mfalme Baasha wa Israeli, walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala.

17. Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala asiingie kwa Asa, mfalme wa Yuda.

18. Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu yote iliyobaki katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu, akawapa watumishi wake, akawatuma Damasko kwa Ben-hadadi mwana wa Tabrimoni, mjukuu wa Hezioni, mfalme wa Aramu, akasema,

19. “Tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama vile walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama, nimekupelekea zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli, ili aache mashambulizi dhidi yangu.”

20. Hapo mfalme Ben-hadadi akakubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao wakateka Iyoni, Dani, Abel-beth-maaka, Kinerethi yote, na nchi yote ya Naftali.

21. Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo aliacha kuujenga mji wa Rama akaishi katika Tirza.

22. Ndipo mfalme Asa alipotoa tangazo kwa watu wote wa Yuda, bila kumwacha hata mtu mmoja, wahamishe mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha mfalme Asa alitumia vifaa hivyo kujengea Geba, katika Benyamini na Mizpa.

23. Matendo mengine yote ya Asa, ushujaa wake na miji yote aliyoijenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Lakini, wakati wa uzee wake, Asa alishikwa na ugonjwa wa miguu.

24. Hatimaye, Asa alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme, katika mji wa Daudi, naye mwanawe Yehoshafati akatawala mahali pake.

Nadabu, mfalme wa Israeli

25. Mnamo mwaka wa pili wa utawala wa Asa huko Yuda, Nadabu, mwana wa Yeroboamu, alianza kutawala huko Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili.

26. Nadabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; akamwiga baba yake ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

27. Baasha mwana wa Ahiya, wa kabila la Isakari, akala njama dhidi ya Nadabu. Basi, wakati Nadabu na jeshi lake walipokuwa wameuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, Baasha akamvamia na kumwua,

28. akatawala mahali pake. Huo ulikuwa mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Asa wa Yuda.

29. Mara tu alipoanza kutawala, Baasha akawaua watu wote wa jamaa ya Yeroboamu; hakuacha hai hata mtu mmoja wa jamaa ya Yeroboamu; hiyo ilikuwa sawa na yale aliyosema Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake, Ahiya wa Shilo.

30. Mambo haya yalifanyika kwa sababu Yeroboamu alimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa dhambi yake na kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

31. Matendo mengine ya Nadabu, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

32. Mfalme Asa wa Yuda na mfalme Baasha wa Israeli walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala.

Baasha, mfalme wa Israeli

33. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya, alianza kutawala Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka ishirini na minne.

34. Baasha alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kutenda dhambi ileile ambayo aliwafanya watu wa Israeli watende.