Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 1:9-23 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Mose akawaambia watu, “Tulipokuwa bado mlimani Sinai, mimi niliwaambieni hivi: ‘Jukumu la kuwaongozeni ni kubwa mno kwangu mimi peke yangu.

10. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya muwe wengi; leo mmekuwa wengi kama nyota za mbinguni.

11. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, na awafanye mzidi kuongezeka mara elfu zaidi ya mlivyo sasa na kuwabariki kama alivyoahidi!

12. Lakini mimi peke yangu nitawezaje kuchukua jukumu hilo zito la kusuluhisha ugomvi wenu?

13. Chagueni kutoka katika kila kabila watu wenye hekima, busara na ujuzi ili niwateue wawe viongozi wenu.’

14. Nyinyi mlikubali, mkanijibu hivi: ‘Jambo ulilosema ni la busara’.

15. Hivyo niliwachukua wale viongozi wenye hekima, busara na ujuzi ambao mliwachagua kutoka katika makabila yenu, nikawaweka kuwa viongozi wenu. Niliwaweka wengine kuwa makamanda wa makundi ya watu elfuelfu, ya watu miamia, ya watu hamsinihamsini na ya watu kumikumi. Nilichagua pia maofisa wengine wa kuchunga kila kabila.

16. “Wakati huohuo niliwapa waamuzi wenu maagizo yafuatayo: ‘Sikilizeni kesi za watu wenu. Toeni hukumu za haki katika visa vya watu wenu, kadhalika na mizozo ya wageni waishio pamoja nanyi.

17. Msimpendelee mtu yeyote katika kutoa hukumu; mtawasikiliza bila upendeleo, wakubwa kwa wadogo. Msitishwe na mtu yeyote, maana hukumu mnayotoa inatoka kwa Mungu. Kesi yoyote ikiwa ngumu zaidi kwenu, ileteni kwangu, nami nitaisikiliza.’

18. Wakati huohuo, niliwaagizeni mambo yote mnayopaswa kufanya.

19. “Basi, kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru, tulianza safari yetu kutoka mlima Horebu, tukapita katika lile jangwa kubwa la kutisha mnalolijua, kwa kufuata njia inayoelekea nchi ya milima ya Waamori. Tulipofika Kadesh-barnea,

20. mimi niliwaambieni: ‘Sasa mmefika katika nchi ya milima ya Waamori ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametupatia.

21. Tazameni, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ameiweka nchi hii mbele yenu. Haya! Ingieni, mkaimiliki kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wenu alivyowaambia. Msiogope wala msifadhaike!’

22. “Kisha nyote mlikuja karibu nami mkaniambia, ‘Tutume watu watutangulie, waipeleleze nchi, halafu warudi kutujulisha njia bora ya kufuata na miji ipi tutaikuta huko.’

23. Jambo hilo lilionekana kuwa jema kwangu, nikawateua watu kumi na wawili, mtu mmoja kutoka katika kila kabila.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 1