Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 20:16-26 Biblia Habari Njema (BHN)

16. “Usimshuhudie jirani yako uongo.

17. “Usiitamani nyumba ya jirani yako, wala mke wake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala chochote kilicho mali ya jirani yako.”

18. Watu waliposikia ngurumo na kuona umeme ukiwaka na kuisikia sauti ya parapanda juu ya mlima uliokuwa unafuka moshi, wote waliogopa na kutetemeka. Wote walisimama mbali,

19. wakamwambia Mose, “Ongea nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza, lakini Mwenyezi-Mungu asiongee nasi, tusije tukafa.”

20. Mose akawaambia, “Msiogope, maana Mungu amekuja kuwajaribu ili mpate kumcha yeye daima na msitende dhambi.”

21. Watu wote walisimama mbali wakati Mose alipokaribia lile wingu zito alimokuwamo Mungu.

22. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli: ‘Mmejionea nyinyi wenyewe kwamba nimeongea nanyi kutoka mbinguni.

23. Mtaniheshimu mimi peke yangu wala msijifanyie miungu ya fedha wala ya dhahabu.

24. Nyinyi mtanijengea madhabahu ya udongo ambayo juu yake mtanitambikia kondoo wenu na ng'ombe wenu kama sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Mahali popote nitakapowakumbusha watu jina langu, papo hapo mimi mwenyewe nitawajia na kuwabariki.

25. Kama mkinijengea madhabahu ya mawe, msiitengeneze kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia vyombo vya kuchongea mawe, mtaitia najisi.

26. Wala msitengeneze madhabahu yenye ngazi za kupandia, mtu asije akauona uchi wa huyo anayepanda juu yake.’

Kusoma sura kamili Kutoka 20