Agano la Kale

Agano Jipya

Methali 16:21-33 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili;neno la kupendeza huwavutia watu.

22. Hekima ni chemchemi ya uhai kwake aliye nayo,bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu.

23. Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara;huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia.

24. Maneno mazuri ni kama asali;ni matamu rohoni na yenye kuupa mwili afya.

25. Mtu aweza kuona njia yake kuwa sawa,lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo.

26. Hamu ya chakula humhimiza mfanyakazi,maana njaa yake humsukuma aendelee.

27. Mtu mwovu hupanga uovu;maneno yake ni kama moto mkali.

28. Mtu mpotovu hueneza ugomvi,mfitini hutenganisha marafiki.

29. Mtu mkatili humshawishi jirani yake;humwongoza katika njia mbaya.

30. Anayekonyeza jicho kwa hila amepanga maovu;anayekaza midomo amekwisha nuia mabaya.

31. Kuwa na mvi za uzee ni taji la utukufu;hupatikana kwa maisha ya uadilifu.

32. Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko mwenye nguvu;aitawalaye nafsi yake ni bora kuliko autekaye mji.

33. Kura hupigwa kujua yatakayotukia,lakini uamuzi ni wake Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili Methali 16