Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 23:29-41 Biblia Habari Njema (BHN)

29. Mtu yeyote asiyefunga siku hiyo ni lazima atengwe mbali na watu wake.

30. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo nitamwangamiza miongoni mwa watu wake.

31. Msifanye kazi: Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu, na katika makao yenu yote.

32. Siku hiyo, itakuwa kwenu Sabato ya mapumziko rasmi na mtafunga. Siku ya Sabato ni siku ya kumi ya mwezi huo tangu jioni hadi jioni inayofuata.”

33. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

34. “Waambie Waisraeli hivi: Tangu siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba. Hiyo ni sikukuu ya Mwenyezi-Mungu.

35. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtakuwa na mkutano mtakatifu na msifanye kazi.

36. Kwa muda wa siku saba mtatoa sadaka anazopewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Siku ya nane mtakuwa na mkutano mkubwa na kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa. Mkutano huo ni mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi.

37. “Hizo ndizo sikukuu za Mwenyezi-Mungu zilizopangwa ambazo mtatoa ilani kuwe na mkutano mtakatifu wa kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka zitolewazo kwa moto, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji, kila moja katika siku yake maalumu.

38. Sadaka hizo ni pamoja na zile mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu siku ya Sabato kama vile pia sadaka zenu za kawaida, sadaka za kutimiza nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu.

39. “Baada ya kuvuna mashamba yenu mtafanya sikukuu kwa muda wa siku saba, tangu siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba. Siku ya kwanza itakuwa siku ya mapumziko na hata siku ya nane.

40. Katika siku ya kwanza mtachukua matunda ya miti yenu mizuri, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi na matawi ya miti iotayo kandokando ya mto, nanyi mtafanya sherehe mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kwa siku saba.

41. Kila mwaka ni lazima kuadhimisha sikukuu hii kwa muda wa siku saba kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu. Mtaifanya katika mwezi wa saba.

Kusoma sura kamili Walawi 23