Agano la Kale

Agano Jipya

Methali 15:4-19 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Ulimi mpole ni chanzo cha uhai,lakini uovu wake huvunja moyo.

5. Mpumbavu hudharau mafundisho ya baba yake,lakini anayekubali maonyo ana busara.

6. Nyumbani mwa mwadilifu mna wingi wa mali,lakini mapato ya waovu huishia na balaa.

7. Mdomo wa mwenye hekima hueneza maarifa,lakini sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu.

8. Sadaka ya waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu,lakini sala ya wanyofu humfurahisha Mungu.

9. Mwenendo wa waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu,lakini Mungu huwapenda wale wafuatao mambo adili.

10. Adhabu kali ipo kwa wanaoacha mwenendo mwema;yeyote achukiaye kuonywa atakufa.

11. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ajua yaliyo Kuzimu na Abadoni,mawazo ya binadamu yatawezaje kujificha mbele yake?

12. Mwenye madharau hapendi kuonywa,hatafuti kamwe maoni ya wenye busara.

13. Moyo wa furaha hungarisha uso,lakini uchungu huvunja moyo.

14. Mwenye busara hutafuta maarifa,lakini wapumbavu hujilisha upuuzi.

15. Kwa mnyonge kila siku ni mbaya,lakini kwa mwenye moyo mchangamfu ni sikukuu.

16. Afadhali kuwa na kidogo na kumcha Mwenyezi-Mungu,kuliko kuwa na mali nyingi pamoja na taabu.

17. Afadhali mlo wa jioni wa mchicha na upendo,kuliko karamu ya nyama nono pamoja na chuki.

18. Mtu wa hasira mbaya husababisha ugomvi,lakini asiye mwepesi wa hasira hutuliza ugomvi.

19. Njia ya mvivu imesambaa miiba,njia ya mwaminifu ni wazi kama barabara kuu.

Kusoma sura kamili Methali 15