Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 19:7-19 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Kama sehemu ya nyama yake italiwa siku ya tatu, tendo hilo ni chukizo; na sadaka hiyo haitakubaliwa,

8. naye atakayekula nyama hiyo ni lazima awajibike kwa uovu wake kwa sababu amekitia unajisi kitu kitakatifu cha Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo atatengwa na watu wake.

9. “Utakapovuna mavuno ya nchi yako, usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba wala usirudi nyuma kukusanya mabaki.

10. Msirudie kukusanya kila kitu katika shamba la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini; utawaachia maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

11. “Msiibe, msidanganye wala kuambiana uongo.

12. Msiape uongo kwa jina langu hata kulikufuru jina la Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

13. “Usimdhulumu jirani yako wala kumwibia. Mshahara wa mtu aliyeajiriwa usikae kwako usiku kucha hadi asubuhi.

14. Usimlaani kiziwi wala kuweka kizuizi mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

15. “Unapotoa hukumu uamue kwa haki; usimpendelee maskini wala kumwogopa mwenye cheo. Bali ni lazima kumwamua jirani kwa haki.

16. Kamwe usipitepite ukiwachongea watu wa jamaa yako. Usiyatie maisha ya jirani yako katika hatari ya kifo kwa maneno yako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

17. “Usimwekee kisasi ndugu yako moyoni mwako, bali upatane daima na jirani yako ili usije ukatenda dhambi.

18. Usijilipize kisasi au kuwa na kinyongo dhidi ya wazawa wa watu wako bali umpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

19. “Yakupasa kuyashika masharti yangu. Usiiache mifugo yako ipandwe na wanyama wa aina nyingine. Shambani mwako usipande mbegu za aina mbili. Usivae vazi lililofumwa kwa aina mbili za nguo.

Kusoma sura kamili Walawi 19