Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 22:9-22 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Kwa hiyo, ni lazima makuhani walishike agizo langu, wasije wakafanya dhambi na kuuawa. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu.

10. “Mtu asiye wa ukoo wa makuhani haruhusiwi kula chakula kitakatifu. Hata mgeni wa kuhani au mwajiriwa wake haruhusiwi kula.

11. Lakini kama kuhani amemnunua mtumwa ili kuwa mali yake, basi, huyo mtumwa anaruhusiwa kula na pia wale waliozaliwa nyumbani kwake.

12. Kama binti yake kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, haruhusiwi kula sadaka ya vitu vitakatifu.

13. Lakini kama binti yake kuhani ni mjane au amepewa talaka na hana mtoto, naye amerudi nyumbani kwa baba yake, akakaa naye kama alipokuwa kijana, basi, anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mgeni haruhusiwi kula vyakula hivyo.

14. Kama mtu mwingine akila vyakula vitakatifu bila kujua, basi, atalipa asilimia ishirini ya thamani ya alichokula na kumrudishia kuhani.

15. Kuhani asivitie unajisi vitu ambavyo Waisraeli wamemtolea Mwenyezi-Mungu

16. na hivyo kusababisha watu wawajibike uovu na hatia yao kwa kula vitu vyao vitakatifu. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayeviweka wakfu vitu hivyo.”

17. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

18. “Mwambie Aroni na wanawe makuhani na Waisraeli wote hivi: Kama mtu yeyote miongoni mwenu au mgeni yeyote aishiye katika Israeli akitoa sadaka yake, iwe ni ya kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari ya kumtolea Mwenyezi-Mungu kwa kuteketezwa,

19. ili apate kukubalika, atatoa katika ng'ombe dume au katika kondoo dume asiye na dosari.

20. Ni marufuku kutoa chochote kilicho na dosari kwani hakitakubaliwa kwa faida yenu.

21. Mtu yeyote anapomtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya amani ili kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari kutoka katika kundi lake la mifugo, ili akubaliwe ni lazima awe ni mnyama mkamilifu; mnyama huyo asiwe na dosari yoyote.

22. Usimtolee Mwenyezi-Mungu mnyama yeyote aliye kipofu, kilema, aliyevunjika mahali, anayetokwa na usaha, mwenye upele au ukurutu, wala usiwatoe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili Walawi 22