Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 6:20-30 Biblia Habari Njema (BHN)

20. “Tangu wakati wa kuwekwa wakfu kwa Aroni na wazawa wake wanapaswa kumtolea Mwenyezi-Mungu kilo moja ya unga laini kwa siku, nusu moja ya unga huo ataitoa asubuhi na nusu nyingine jioni.

21. Unga huo utachanganywa na mafuta na kuokwa; kisha utauleta ukiwa vipandevipande na kumtolea Mwenyezi-Mungu; na harufu ya sadaka yake itampendeza Mungu.

22. Kuhani aliye mzawa wa Aroni ambaye amepakwa mafuta kushika nafasi yake atamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka hiyo; hilo ni agizo la milele. Sadaka yote itateketezwa.

23. Sadaka yoyote ya nafaka iliyotolewa na kuhani itateketezwa yote; haitaliwa kamwe.”

24. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

25. “Mwambie Aroni na wanawe kuwa ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuondoa dhambi, mahali pale ambapo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa ndipo atakapochinjiwa mnyama wa sadaka ya kuondoa dhambi, mbele ya Mwenyezi-Mungu; hiyo ni sadaka takatifu kabisa.

26. Kuhani anayetolea sadaka hiyo ndiye atakayeila. Italiwa mahali patakatifu, uani mwa hema la mkutano.

27. Chochote kitakachogusa nyama hiyo kitakuwa kitakatifu; vazi lolote likidondokewa na damu ya sadaka hiyo, basi, vazi hilo litaoshewa mahali patakatifu.

28. Sadaka hiyo ikichemshiwa katika vyombo vya udongo, vyombo hivyo vitavunjwa. Lakini ikiwa vyombo hivyo ni vya shaba, basi, vitasafishwa na kusuzwa kwa maji.

29. Wanaoruhusiwa kuila ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao kwa vile hiyo ni sadaka takatifu kabisa.

30. Lakini kama damu ya sadaka yoyote ya kuondoa dhambi imeletwa ndani ya hema la mkutano ili kufanyia ibada ya upatanisho katika mahali patakatifu, sadaka hiyo itateketezwa kwa moto.”

Kusoma sura kamili Walawi 6