Agano la Kale

Agano Jipya

Zekaria 14:9-18 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye mfalme pekee wa dunia yote; naye atakuwa ndiye Mwenyezi-Mungu pekee, mmoja tu, na jina lake litakuwa ndilo jina pekee.

10. Nchi yote, tangu Geba hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itageuzwa kuwa mbuga tambarare kabisa. Lakini mji wa Yerusalemu utabaki juu mahali pake tokea lango la Benyamini mpaka lango la zamani, hadi kwenye lango la Konani, tangu mnara wa Hanareli hadi kwenye mashinikizo ya mfalme.

11. Mji wa Yerusalemu utakaliwa na watu kwani ndani yake haitakuwapo laana tena; naam, watu watakaa humo kwa usalama.

12. Lakini kuhusu wale watu ambao walikuja kupigana na Yerusalemu, haya ndiyo maafa ambayo Mwenyezi-Mungu atawaletea: Miili yao itaoza wangali hai; macho yao yataoza yakiwa kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza zikiwa vinywani mwao.

13. Siku hiyo, hofu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu itawakumba watu, na kila mtu atamshambulia mwenzake.

14. Watu wa Yuda watapigana kuulinda mji wa Yerusalemu; utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka nchi ya Yuda utakusanywa: Watakusanya dhahabu, fedha na mavazi kwa wingi sana.

15. Maafa makubwa yatawakumba farasi, nyumbu, ngamia, punda na wanyama wote watakaokuwamo katika kambi hizo za maadui.

16. Kisha, kila mtu aliyesalimika kati ya mataifa yote yaliyokuja kuushambulia mji wa Yerusalemu, atakuwa akija Yerusalemu mwaka hata mwaka, kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, na kuadhimisha sikukuu ya vibanda.

17. Iwapo taifa lolote duniani halitakwenda Yerusalemu kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, basi, mvua haitanyesha katika nchi yao.

18. Iwapo Wamisri watakataa kuiadhimisha sikukuu ya vibanda, basi, Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa ugonjwa uleule atakaowapiga nao mataifa yote yanayokataa kuiadhimisha sikukuu hiyo.

Kusoma sura kamili Zekaria 14