Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28

Agano la Kale

Agano Jipya

Mathayo 22 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfano wa karamu ya harusi

1. Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano:

2. “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi.

3. Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika.

4. Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’

5. Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake,

6. na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua.

7. Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao.

8. Kisha akawaambia watumishi wake: ‘Karamu ya harusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili.

9. Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje harusini.’

10. Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya harusi ikajaa wageni.

11. “Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya harusi.

12. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya.

13. Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’”

14. Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.”

Kulipa kodi kwa Kaisari

15. Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake.

16. Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako.

17. Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?”

18. Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu?

19. Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha.

20. Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?”

21. Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.”

22. Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.

Suala juu ya ufufuo

23. Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu.

24. Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto.

25. Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane.

26. Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba.

27. Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama.

28. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.”

29. Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu.

30. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni.

31. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia,

32. ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”

33. Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.

Amri kuu

34. Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja.

35. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu,

36. “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?”

37. Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’.

38. Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza.

39. Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’.

40. Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili.”

Suala juu ya Kristo

41. Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza,

42. “Nyinyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Wa Daudi.”

43. Yesu akawaambia, “Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema:

44. ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:Keti upande wangu wa kulia,mpaka niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.’

45. Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo ‘Bwana,’ anawezaje kuwa mwanawe?”

46. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.