Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31

Agano la Kale

Agano Jipya

Methali 14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake,lakini mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

2. Mwenye mwenendo mnyofu humcha Mwenyezi-Mungu,lakini mpotovu humdharau Mungu.

3. Mpumbavu hujiadhibu mwenyewe kwa kuropoka kwake,lakini mwenye hekima hulindwa na maneno yake.

4. Bila ng'ombe wa kulima ghala za mtu ni tupu,mavuno mengi hupatikana kwa nguvu ya ng'ombe wa kulima.

5. Shahidi mwaminifu hasemi uongo,lakini asiyeaminika hububujika uongo.

6. Mwenye dharau hutafuta hekima bure,lakini mwenye busara hupata maarifa kwa urahisi.

7. Ondoka mahali alipo mpumbavu,maana hapo alipo hamna maneno ya hekima.

8. Hekima ya mwenye busara humwonesha njia yake,lakini upumbavu wa wapumbavu huwadanganya wenyewe.

9. Wapumbavu huchekelea dhambi,bali wanyofu hupata fadhili kwa Mungu.

10. Moyo waujua uchungu wake wenyewe,wala mgeni hawezi kushiriki furaha yake.

11. Nyumba ya mtu mwovu itabomolewa,lakini hema ya wanyofu itaimarishwa.

12. Njia unayodhani kuwa ni sawa,mwishoni yaweza kukuongoza kwenye kifo.

13. Huzuni yaweza kufichika katika kicheko;baada ya furaha huja majonzi.

14. Mtu mpotovu atavuna matunda ya mwenendo wake,naye mtu mwema atapata tuzo la matendo yake.

15. Mjinga huamini kila kitu anachoambiwa,lakini mwenye busara huwa na tahadhari.

16. Mwenye hekima ni mwangalifu na huepa uovu,lakini mpumbavu hajizuii wala hana uangalifu.

17. Mwenye kuwaka hasira haraka hutenda kipumbavu,lakini mwenye busara ana uvumilivu.

18. Wajinga hurithi upumbavu,lakini wenye busara hutuzwa taji ya maarifa.

19. Waovu watapiga magoti mbele ya watu wema,watu wabaya mlangoni mwa waadilifu.

20. Maskini huchukiwa hata na jirani yake,lakini tajiri ana marafiki wengi.

21. Anayemdharau jirani yake ni mwenye dhambi,bali ana heri aliye mwema kwa maskini.

22. Anayepanga maovu kweli anakosea!Wanaopanga kutenda mema hufadhiliwa.

23. Bidii katika kila kazi huleta faida,lakini maneno matupu huleta umaskini.

24. Mali ni taji ya fahari ya wenye hekima,lakini ujinga ni shada la wapumbavu.

25. Shahidi wa kweli huokoa maisha,lakini msema uongo ni msaliti.

26. Amchaye Mwenyezi-Mungu ana tumaini imara,na watoto wake watapata kimbilio salama.

27. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni chemchemi ya uhai;humwezesha mtu kuepa mitego ya kifo.

28. Fahari ya mfalme ni wingi wa watu wake,lakini bila watu mtawala huangamia.

29. Mtu asiye mwepesi wa hasira ana busara kubwa,lakini akasirikaye upesi hukuza upumbavu.

30. Amani rohoni humpa mtu afya,lakini tamaa huozesha mifupa.

31. Anayemdhulumu maskini anamtukana Muumba wake,lakini amwoneaye huruma mhitaji anamtukuza Mungu.

32. Mwovu huangamizwa kwa matendo yake maovu,lakini mwadilifu hupata usalama kwa unyofu wake.

33. Hekima imo moyoni mwa mtu mwenye busara;haipatikani kamwe mioyoni mwa wapumbavu.

34. Uadilifu hukuza taifa,lakini dhambi ni balaa kwa taifa lolote.

35. Mfalme humfadhili mtumishi atendaye kwa hekima,lakini hasira yake huwakumba watendao yasiyofaa.