Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31
  32. 32
  33. 33
  34. 34
  35. 35
  36. 36
  37. 37
  38. 38
  39. 39
  40. 40
  41. 41
  42. 42
  43. 43
  44. 44
  45. 45
  46. 46
  47. 47
  48. 48
  49. 49
  50. 50
  51. 51
  52. 52
  53. 53
  54. 54
  55. 55
  56. 56
  57. 57
  58. 58
  59. 59
  60. 60
  61. 61
  62. 62
  63. 63
  64. 64
  65. 65
  66. 66

Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 37 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme anaomba shauri kwa nabii Isaya

1. Basi, mfalme Hezekia aliposikia habari hiyo alirarua mavazi yake, akavaa vazi la gunia, akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

2. Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia.

3. Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa, na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama anayetaka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa.

4. Inawezekana kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya mkuu wa matowashi ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atapinga maneno aliyoyasikia; kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”

5. Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya,

6. yeye akawaambia, “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Usiogope kwa sababu ya maneno ya watumishi wa mfalme wa Ashuru uliyoyasikia, maneno ambayo wameyasema kunidharau.

7. Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi halafu atarudi katika nchi yake, na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”

Waashuru wanatishia tena

8. Kisha yule mkuu wa matowashi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akishambulia mji wa Libna.

9. Halafu aliposikia habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema,

10. “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru.

11. Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, unadhani wewe utaokoka?

12. Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo wazee wangu waliyaangamiza?

13. Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na Iva?’”

14. Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu.

15. Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema;

16. “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, unayeketi katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa. Wewe ndiwe uliyeumba mbingu na dunia.

17. Ee, Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka na kukutukana wewe Mungu uliye hai.

18. Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa yote na nchi zao.

19. Waliweza kuitupa miungu yao motoni, kwa sababu haikuwa miungu kweli bali sanamu za miti au mawe zilizochongwa na mikono ya watu.

20. Sasa ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utuokoe makuchani mwa Senakeribu, ili falme zote za dunia zijue kwamba wewe peke yako ndiwe uliye Mwenyezi-Mungu.”

Ujumbe wa Isaya kwa mfalme

21. Kisha Isaya mwana na Amozi, alituma ujumbe kwa Hezekia akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: Kwa kuwa umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru,

22. basi huu ndio ujumbe wangu kuhusu huyo mfalme:Mji wa Siyoni, naam, Yerusalemu,unakudharau na kukutukana.Yerusalemu, mji mzuriunakutikisia kichwa kwa dhihaka.

23. Wewe umemtukana nani?Umemkashifu nani?Umethubutu kumbeza nani kwa majivuno?Ni mimi Mungu, Mtakatifu wa Israeli!

24. Umewatumia watumishi wako kunidhihaki mimi Bwana;wewe umesema, ‘Kwa magari yangu mengi ya vita,nimekwea vilele vya milima,mpaka kilele cha Lebanoni.Nimeangusha mierezi yake mirefu,na misonobari mizurimizuri.Nimevifikia vilele vyakena ndani ya misitu yake mikubwa.

25. Nimechimba visima na kunywa maji yake,na nilikausha vijito vya Misrikwa nyayo za miguu yangu.’

26. “Je, hujasikia ewe Senakeribu kwambanilipanga jambo hili tangu zamani?Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.Nilikuweka uifanye miji yenye ngomekuwa rundo la magofu.

27. Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu,wametishika na kufadhaika.Wamekuwa kama mimea shambani,kama nyasi changa shambani,kama majani yaotayo juu ya paaau kama ngano kabla hazijakomaaambazo hunyauka upepo mkavu uvumapo.

28. Lakini, nakujua wewe Senakeribu;najua kila unachofanya na kuacha kufanya;najua mipango yako dhidi yangu.

29. Kwa vile umefanya mipango dhidi yanguna nimeusikia ufidhuli wako,nitatia ndoana yangu puani mwako,na lijamu yangu kinywani mwako.Nitakurudisha njia ileile uliyojia.”

30. “Na hii ndiyo itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake.

31. Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu.

32. Maana kutakuwa na watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amedhamiria kukamilisha hayo.

33. Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu, wala kuupiga mshale wala kuingia kwa ngao wala kuuzingira.

34. Atarudi kwa njia ileile aliyojia na wala hataingia katika mji huu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimetamka hayo.

35. Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuuokoa mji huu.”

36. Basi, wakati wa usiku malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu 185,000. Halafu kulipopambazuka watu hao wote walionekana wakiwa maiti.

37. Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda kwake, akakaa Ninewi.

38. Siku moja, wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri, walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe, akatawala badala yake.